Madhara apatayo mtoto kwa mama mjamzito kulala chali

08:39
Wana AfyaJamii Wanawake wajawazito wanaopenda kulala chali  wapo kwenye hatari  ya kuzaa mtoto mfu(stillbirth),kulingana na wanasayansi.
Katika utafiti  uliofanyika nchini Ghana, wanawake wajawazito ambao walipenda kulala chali wakati wa ujauzito  walikuwa  kwenye hatari mara tano zaidi ya kuzaa watoto wenye uzito mdogo na  kwa wanawake wengine walizaa watoto wafu.

Utafiti huu ulifanyika nchini Ghana kutokana na kuwa kati ya watoto 1000 wanaozaliwa 20 hadi 50 kati yao huwa ni watoto wafu.Hata hivyo, utafiti mpya uliofanyika nchini New Zealand pia umehusisha kulala chali kwa mwanamke mjamzito na idadi kubwa ya  watoto wafu wanaozaliwa  katika nchi zenye raia wenye kipato kikubwa.

Mkuu wa utafiti huu,Louise O'Brien  kutoka chuo kikuu cha Michigan, nchini Marekani amesema kama kutokulala chali wakati wa ujauzito hupunguza uwezekano wa kuzaa mtoto mfu basi ni vizuri kuhamasisha kina mama wajawazito kutolala chali kwani hii ni njia rahisi na isiyokuwa na gharama yoyote ile.
Tabia hii ya kulala chali wakati wa ujauzito inaweza kuepukika kwa kuwashauri  kina mama wajawazito madhara yanayopatikana kwa kulala chali.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha ya kwamba zaidi ya robo ya idadi ya watoto wanaozaliwa wafu inaweza kuepukika kwa kubadilisha staili ya kulala tu kwa wanawake wajawazito.


Siku zote madaktari wanashauri kina mama wajawazito kulala ubavu mmoja hasa upande wa kushoto ili kuepuka kuzaa mtoto mfu au mtoto mwenye uzito mdogo kwa sababu mwanamke mjazito anapolalia ubavu wake wa kushoto huongeza mzunguko wa damu kwa kiumbe kilichomo ndani yake.

          Utafiti huu uliofanyika nchini Ghana unaunga mkono utafiti uliofanyika hivi karibuni nchini Australia unaojulikana kama Sydney Stillbirth Study ambao ulisema ya kwamba wanawake wanaolala chali wakati wa ujauzito wako kwenye hatari ya mara sita zaidi ya kuzaa watoto wafu.Utafiti huu wa Australia ulifanyika kwa miaka mitano na ulihusisha wanawake wajawazito 295 kutoka katika hospitali nane nchini Australia.

Naye mtafiti mkuu katika utafiti huu Dr. Adrienne Gordon, kutoka Sydney's Royal Prince Alfred Hospital amesema “Tafiti za awali zilionyesha ya kwamba wanawake wanaolala chali wakati wa ujauzito, hupunguza mzunguko wa damu unaotakiwa kwenda kwa mtoto.Lakini  pia ni vizuri kwa wanawake ambao ni wajawazito  kutotaharuki kama wakati mwingine watalala chali.’’Kutokana na idadi ndogo ya wanawake wajawazito waliohusishwa kwenye utafiti huu sisi wana Tanzmed tunachelea kusema ya kwamba ni vigumu kusema utafiti huu umetoa mapendekezo sahihi ya  namna ya kulala kwa wanawake wajawazito.

Pia kutokana na kutoangalia muda ambao wanawake hao walilala wakiwa chali (mfano kama walilala masaa 4,6 au 8 kwa siku na kwa siku ngapi) na tofauti ya hatari kati ya wanawake wajawazito waliolala muda mfupi na mrefu, hivyo tunawaambia wanawake wajawazito kutohofu kama watalala chali lakini ni bora kuchukua tahadhari mapema.Tafiti hii inatoa changamoto kwa watafiti wetu wa afya kuangalia jinsi ya kufanya tafiti kama hizi katika mazingira ya kwetu.Baadhi ya milalo salama kwa mama mjamzito ni kulalia ubavu wa kushoto kama nilivyoonesha hapa chini kwenye picha:





Share this

Related Posts

First