Maumivu Wakati Wa Kukojoa

10:12 Add Comment
Maumivu wakati wa kukojaoa ni hali inayotokea kwa watu wengi ikisababishwa na magonjwa mbalimbali. Maumivu wakati wa kukojoa hujulikana kwa kitaalamu kama dysuria. Kati ya sababu kuu zinazosababisha maumivu wakati wa kukojoa ni maambukizi ya mfumo wa mkojo (Urinary tract Infection – UTI) hasa kwa wanawake na magonjwa ya zinaa

Maumivu Wakati wa Kukojoa Yanavyotokea 

Maumivu wakati wa kukojoa hutokana na kuchubuka kwa njia ya mkojo. Kuchubuka huku hutokea pale njia ya mkojo inaposhambuliwa na bakteria au kemikali na kuharibu ukuta wa juu wa njia ya mkojo hivyo huwa kama kidonda. Pale mkojo unapopita eneo hili basi unapata maumivu kama ya kuungua. Maumivu haya yanaweza kutokea wakati wote unakojoa, mwanzoni au mwishoni mwa kukojoa.

Kwa watoto wadogo, mara nyingi hulia wakati wanakojoa ikiwa wanapata maumivu kwani hawawezi kuongea.

Pia yanaweza kuambatana na dalili nyingine kama homa, kutokwa na usaha au uchafu sehemu za siri, kutokwa mkojo wenye damu damu, maumivu chini ya kitovu au maumivu ya ubavu (flanks).

Sababu za Maumivu Haya

Maumivu haya hutegemea na chanzo cha ugonjwa unaoleta dalili hii. Baadhi ya vyanzo vya maumivu wakati wa kukojoa ni:

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

Ugonjwa huu huleta maumivu kama ya kuungua kwenye njia ya mokojo. Pia maumivu yanaweza kufika mpaka chini ya kitovu wakati wa kukojoa. Dalili nyingine zinazoweza kuambatana na hali hii ni homa, kukojoa mara kwa mara, kuhisi mkojo hauishi kwenye kibofu na maumivu ya mgongo.

Magonjwa ya zinaa

Magonjwa ya zinaa kama kisonono na klamidia huleta maumivu wakati wa kukojoa hasa kwa wanaume, maumivu haya huwa kama ya kuungua wakati mkojo unatoka. Dalili nyingine zinazoweza kuambatana na magonjwa haya ni kutoa uchafu kama usaha sehemu za siri, maumivu chini ya kitovu na homa.

Kichocho

Kichocho husababisha maumivu wakati wa kukojoa ikiambatana na kutoa mkojo wenye damu.

Magonjwa mengine yanayoweza kusababisha maumivu wakati wa kukojoa ni:
  • Mawe ya Figo (kidney stones)
  • Maambukizi ya ukeni (vaginitis)
  •  Saratani ya kibofu cha mkojo
  •  Kuchubuka kwa njia ya mkojo kutokana na ajali, kupigwa, kuendesha farasi au mazoezi mengine.
  •  Kuwekewa mpira wa mkojo (urinary catheter) au kuingizwa vipimo vya njia ya mkojo au kibofu (instrumentation of urethra or bladder).

vipimo

Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika ili kujua chanzo cha maumivu wakati wa kukojoa.

  •  Kipimo cha uchunguzi wa mkojo (urinalysis)
  •  Kuotesha mkojo (urine culture)

Uchunguzi za mkojo na kuotesha mkojo huweza kuonesha kama kuna maambukizi kwenye njia ya mkojo. Pia mabaki ya mawe ya figo huweza kuonekana.

  •     Kipimo cha Ultrasound ya tumbo na kiuno (Pelvic and abdominal ultrasound).
Kipimo hiki huweza kuonesha matatizo ya kwenye figo ikiwemo mawe ya figo, uvimbe kwenye mfumo ya mkojo au maambukizi ya figo. Vipimo vingine kama X-ray au CT Scan vinaweza kufanyika kama dalili nyingine zikiashiria hivyo.

Matibabu

Maumivu wakati wa kukojoa ni dalili, hivyo matibabau huelekezwa kwa ugonjwa unaoleta tatizo hili. Maumivu haya yanaweza kutibiwa na kupona kabisa. Ikiwa mtu atapata tena maambukizi yaliyoleta dalili hii awali, basi maumivu haya yanaweza kujirudia tena.

Wahi kwenye kituo cha kutoa huduma za afya uonapo dalili kama hii haraka. Endapo dalili nyingine zinatokea kama damu kwenye mkojo, homa au maumivu ya kwenye ubavu usipoteze muda

Dawa Ya Misoprostol

00:01 Add Comment
Misoprostol ni dawa iliyo kundi la prostaglandin. Hujulikana kwa majina kama miso, cytotec. Hutumika katika matibabu ya vidonda vya tumbo, ujauzito na wakati wa kujifungua. Inatumika sana katika utoaji mimba usio salama na wakati mwingine kuleta madhara kama kutokwa damu nyingi na maambukizi kwenye mji wa uzazi.

Namna Inavyofanya kazi

Misoprostol ni aina ya prostagndin ya kutengenezwa ambayo huzuia kuzalishwa kwa tindikali ya tumboni na kusaidia kulinda kuta za tumbo. Kwenye tumbo la uzazi hufanya kuta za uzazi kusinyaa na hivyo mimba kutoka kama mtu alikuwa mjamzito, au damu kutoka kama alikuwa amejifungua.

Matumizi

Hupatikana  katika vidonge vya mikrogramu 100 na 200 (100 and 200 microgram). Vidonge hivi unaweza kunywa, kuweka chini ya ulimi au ndani ya uke ikitegemea na tatizo linalotibiwa. Dawa hii hutumika katika;

  • Kutibu vidonda vya tumbo kutokana na dawa za NSAID.
  • Kutoa mimba.
  • Kuanzisha uchungu wakati wa kujifungua
  • Kuzuia kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua

Usalama Wakati Wa Ujauzito

Misoprostol sio salama kabisa kutumika wakati wa ujauzito. Inaharibu mimba.

Tahadhari

Usitumie dawa hii kama una mimba. Inaweza kuharibu ujauzito wako.
Usitumi dawa hii na dawa zenye magneziamu (magnesium) kama antacids.
Kama unatarajia kuwa na ujauzito, mwelezee daktari wako kabla ya kuanza kutumia dawa hii.
Usiache dawa bila kushauriana na daktari wako.
Usinywe pombe wakati unatumia dawa hii.

Madhara

Matumizi ya misoproatol yanaweza kuleta madhara yafuatayo kwa mtumiaji.

  • Kuharisha
  • Tumbo kuuma
  • Kichwa kuuma
  • Kichefuchefu
  • Tumbo kujaa gesi
  • Kutapika
  • Mabadiliko katika hedhi
  • Kupasuka mji wa uzazi

Wahi hospitali kama unatokwa na damu ukeni baada ya kunywa dawa hii.

Kunywa dawa pamoja na chakula ili kuondoa uwezekano wa kuharisha.

Vyakula Vinavyofaa Kwa Mjamzito

23:13 Add Comment

Lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana, kwani lishe hii hutumika kwa mama na mtoto anaendelea kukua tumboni. Kwa kawaida mahitaji ya chakula na virutubisho mwilini mwa mwanamke huongezeka wakati wa ujauzito na kadri ujauzito unavyoendelea kukua, virutubisho hivyo hutumika kujenga mwili wa mama na mtoto. Hivyo maamuzi ya lishe au lishe mama anayopata huathiri pia maendeleo ya mtoto anayekua mwilini mwake. Tutaona vyakula muhimu vya kuzingatia lishe bora wakati wa ujauzito na baadhi ya vitu vya kukwepa. Mlo kamili (balanced diet), ni muhimu kwa ajili ya maendeleo mazuri ya afya ya mjamzito na mtoto tumboni. Pamoja na mlo kamili mjamzito hupewa virutubisho ziada (supplements) kwa ajili ya kuongeza madini kama ya chuma na Foliki. Mlo kamili unajumuisha vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamini, madini na maji kama inavyochambuliwa hapa chini

Nafaka na Vyakula vya Wanga.

Vyakula hivi huupa mwili nguvu za kufanya kazi ikiwemo ukuaji wa mtoto tumboni. Vyanzo vya wanga ni kama nafaka mbalimbali(mahindi,mtama,ulezi n.k), viazi, ndizi, mihogo. Ni vizuri mjamzito awe anapata nafaka kamili(whole grains) kama mahindi, ngano na mchele usiokobolewa; cereals n.k.

Nyama, Samaki na Vyakula vya Protini.

Hivi ni muhimu kwenye kuujenga mwili, hasa kipindi cha miwezi wa 4 mpaka wa 9 ambacho viungo mbalimbali vya mtoto vinajengwa. Ni muhimu mama apate vyakula vya protini vya kutosha ili kuhakikisha ukuaji wa mtoto unaenda vizuri. Nyama za kuku, ng’ombe, mbuzi, senene, panzi na wanyama wengine ; vyanzo vya protini za mimea kama maharage, soya, njugu, njegere, karanga,korosho n.k . Samaki, maziwa, mayai ni vyanzo vingine vya protini muhimu.

Vyakula vya Mafuta.

Hutumika kwenye kuupatia mwili nguvu pamoja na ujengaji wa seli za mwili. Mara nyingi vyakula kama nyama, karanga, ufuta, alizeti,senene, panzi, samaki na matunnda kama maparachichi huwa na mafuta. Ni vizuri kutumia mafuta yatokanayo na mimea ili kupunguza mafuta yenye lehemu(cholesterol) nyingi.

Mboga za Majani na Matunda.

Matunda na mboga za majani ni sehemu muhimu sana ya mlo wakati wa ujauzito, kwani huupatia mwili vitamini, madini na kambakamba kwa ajili ya kulainisha chakula. Vitamini husaidia kuimarisha kinga ya mwili sambamba na ufanyaji kazi wa mwili.  Madini kama ya chuma, kalsiamu, zinki, madini joto(Iodine) na magneziamu ni muhimu kwa ukuaji salama wa mtoto tumboni mwa mama.

Vitamini B9 (Foliki asidi) na madini ya chuma hutolewa kama virutubisho ziada kliniki wakati wa ujauzito ili kutosheleza mahitaji ya mwili na kuzuia hatari ya upungufu wa damu kutokea.

Maji

Maji ni muhimu kwenye mmenyenyo na unyonywaji wa chakula, pia husaidia kuzuia choo kigumu, mwili kuvimba na maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI). Inashauriwa mjamzito anywe maji si chini ya lita 2.3 kwa siku, yanaweza kuwa katika chai, juisi, soda, au maji yenyewe. Ni vema zaidi kama akinywa maji kama maji zaidi na kupunguza vinywaji kama soda.

Mfano wa Mpangilio wa Mlo.

Ili kuhakikisha mlo kamili mjamzito anaweza kufuata mfano wa mpangilio wa mlo ufuatao;

Mfano,
Mlo wa Asubuhi:    A – Chungwa/ Embe/ Ndizi mbivu/ Parachichi,  B – Mkate/ Maandazi/ Chapati/ Vitumbua,Uji      C – Karoti    D – Mayai,    E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya  Soya
Mlo wa Mchana:     A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na chungwa,  B – Ugali/ Wali/ Ndizi/ Makande/ Tambi          C – Mchicha/ matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji,      D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa        E – Maziwa/ Mtindi/ Siagi/ Maziwa ya  Soya.
Mlo wa Usiku:        A – Parachichi/ Papai/ Ndizi/ Embe na Chungwa,   B – Wali/ Ndizi/ Viazi/ Tambi/ Chapati          C – Mchicha/ Matembele/ Mnavu/ Kisamvu/ Spinach/ Kabeji,      D – Maharage/ Samaki/ Kuku/ Njugu/ Nyama/ Dagaa           E – Maziwa/Mtindi/Siagi/Maziwa ya  Soya.

Vitu na Vyakula vya kuepuka/kupunguza

Matumizi ya Pombe wakati wa ujauzito huathiri mtoto. Haishauriwi kutumia pombe kabisa!
Uvutaji Sigara
Kupunguza unywaji wa kahawa au vinywaji vyenye caffeine nyingi.
Samaki aina ya papa, swordfish, tilefish na king mackerel kwani wana mekuryi kwa wingi amabayo ni mbaya kwa afya.