Tatizo la kukosa hedhi au amenorrhea linaweza kutokea awali kabisa (primary) au baadaye kabisa maishani (secondary).
Primary amenorrhea ni hali ya kukosa hedhi inayoweza kumtokea msichana aliye katika umri wa kuvunja ungo na ambayo huweza kuendana na hali ya kukosa mabadiliko ya kubalehe kama vile kuota matiti au nywele za kinena; au msichana anaweza kuwa na mabadiliko ya kubalehe lakini asipate hedhi.
Secondary amenorrhea ni hali ya kukosa hedhi inayomtokea mwanamke ambaye si mjamzito, hanyonyeshi, na ambaye hajavuka umri wa kukosa hedhi (menopause) na wala hatumii njia za uzazi wa mpango kama vile sindano au vidonge, na ambaye hapo awali alikuwa akipata hedhi kama kawaida lakini akasimama kwa miezi mitatu au zaidi.
Mwanamke hupataje hedhi?
Ili mwanamke aweze kuwa na mzunguko ulio sahihi wa hedhi, ni lazima matezi yake ya hypothalamus napituitary pamoja na kiwanda cha kutengeneza mayai ya kike (ovaries) na mji wa mimba (uterus) vifanye kazi zake sawasawa.
Hypothalamus huchochea tezi la pituitary kuzalisha hormone chochezi ya follicle au follicle-stimulating hormone (FSH) pamoja na homoni ya luteinizing (LH). Hizi FSH na LH kwa pamoja huchochea ovarieskuzalisha homoni za estrogen pamoja na progesterone. Kazi za estrogen na progesterone ni kusababisha mabadiliko katika ukuta wa uterus yaani endometrium ikiwepo kupata hedhi. Ili damu ya hedhi iweze kutoka nje, njia ya uzazi ya mwanamke haina budi kuwa huru yaani isiyo na matatizo yeyote yale.
Amenorrhea husababishwa na nini?
Visababishi vya amenorrhea vyaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu, vile vinavyohusisha matatizo katika mfumo wa homoni, vile vinavyohusisha matatizo ya kimaumbile katika njia ya uzazi ya mwanamke na vile vinavyohusisha mabadiliko katika mwili wa mwanamke.
1. Matatizo katika mfumo wa homoni: Matatizo katika mfumo wa homoni yanaweza kuwa katika tezi za hypothalamus, pituitary au ovary.
1. Matatizo katika Hypothalamus: Matatizo katika hypothalamus yanayoweza kusababisha mwanamke kukosa hedhi ni pamoja na
§ Uvimbe katika ubongo karibu na tezi ya pituitary
§ Ukosefu au upungufu wa homoni zinazochochea kukua na kufanya kazi kwa via vya uzazi. Ugonjwa huu hujulikana kama Kallmann syndrome
§ Lishe duni na utapia mlo
§ Uzito mdogo kuliko kawaida (kukonda kwa kupitiliza)
2. Matatizo katika tezi ya Pituitary: Vyanzo vinavyohusisha tezi ya pituitary ni pamoja na
§ Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni ya prolactin katika damu au kwa kitaalamuProlactinemia. Prolactin ni homoni inayochochea uzalishaji wa maziwa wakati wa kunyonyesha. Hali ya kuwa na prolactin nyingi katika damu inaweza kutokea iwapo kuna uvimbe unaoitwa (prolactinoma) katika tezi ya pituitary.
§ Kuwepo kwa uvimbe mwingine wowote katika tezi ya pituitary.
§ Pituitary kushindwa kufanya kazi baada ya seli zake kufa, hususani iwapo mama alipoteza damu nyingi wakati wa kujifungua.
§ Kuharibika kwa tezi ya pituitary baada ya seli zake kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili.
§ Kuwa na historia ya kupata tiba ya mionzi inayohusisha tezi ya pituitary.
3. Matatizo katika ovary: Vyanzo vinavyohusisha matatizo katika viwanda vya kuzalisha mayai ya kike yaani ovaries ni pamoja na
§ Kutozalishwa kabisa kwa mayai (Anovulation)
§ Kuwepo kwa kiwango kingi cha homoni za kiume katika damu (Hyperandrogenemia)
§ Ovary kuwa na vifukovifuko (Polycystic ovarian syndrome) na kushindwa kufanya kazi zake vizuri. Haya ni matatizo ya homoni ambayo huwapata baadhi ya wanawake walio katika umri wa kuzaa
§ Kufa na kushindwa kufanya kazi kwa ovary kabla ya muda wake
§ Ugonjwa wa kuzaliwa unaoitwa Turner syndrome ambao humbatana na kukosekana kwa ovary au ovary kuwa changa kuliko kawaida, msichana kushindwa kuvunja ungo na msichana kuwa na kimo kifupi kuliko kawaida. Ugonjwa huu hutokana na matatizo ya kijenitikia (genetic disease)
§ Ukosefu wa kimaumbile wa ovary ambao hutokea wakati wa ukuaji
§ Kufa kwa ovary baada ya seli zake kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili
§ Historia ya kuwahi kupata tiba ya mionzi au madawa yanaathiri ovary
§ Ugonjwa wa kurithi wa Galactosemia unaoambatana na kuwa na kiwango cha juu cha sukari aina ya galactose katika damu
2. Matatizo ya kimaumbile katika njia ya uzazi: Matatizo ya kimaumbile katika njia ya mfumo wa uzazi wa mwanamke yanayoweza kusababisha ukosefu wa hedhi ni pamoja na
1. Mwanamke/msichana kuzaliwa bila kuwa na uke, shingo ya uzazi au mji wa mimba (uterus)
2. Kuta za uterus zinazotazamana kujishikiza pamoja
3. Utando unaozunguka uke (hymen) kuziba kabisa na kukosekana kwa tundu la kupitishia damu ya hedhi (imperforate hymen)
4. Kuwepo kwa utando unaokatiza katika uke unaozuia damu ya hedhi kushindwa kutoka
3. Mabadiliko katika mwili wa mwanamke: Mambo yanayoweza kuathiri mwili wa mwanamke na kumfanya ashindwe kupata hedhi ni pamoja na
1. Kula kiasi kidogo sana cha chakula kuliko kawaida au kula kupita kiasi
2. Unene uliopitiliza au kupungua uzito/kukonda isivyo kawaida
3. Uwepo wa magonjwa sugu kama kifua kikuu
4. Utapiamlo
5. Msongo wa mawazo
6. Matumizi ya madawa ya kulevya
7. Matumizi ya baadhi ya madawa hususani baadhi ya dawa za kutibu magonjwa ya akili
8. Kuwa na hofu iliyopitiliza
9. Kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi
Dalili za Amenorrhea ni zipi?
Kukosa hedhi siyo ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo kwa tatizo au ugonjwa fulani katika mwili. Kulingana na ugonjwa unaosababisha tatizo hili, kukosa hedhi kunaweza kuambatana pia na
· Matiti kutoa maziwa wakati mwanamke si mjamzito na wala hanyonyeshi, maumivu ya kichwa na matatizo katika kuona vitu ambavyo kwa pamoja vinaweza kuashiria uwepo wa uvimbe katika ubongo
· Mwanamke kuwa na nywele na vinyweleo vingi mwilini na kuota ndevu kama mwanaume hali inayoashiria kuwepo kwa wingi kwa homoni za kiume za androgen
· Ukavu katika uke, kutoka jasho sana wakati wa usiku, au mabadiliko katika kupata usingizi vinaweza kuashiria matatizo katika ovary
· Kuongezeka uzito kupita kiasi au kupungua kwa uzito isivyo kawaida
· Mwanamke kuwa na mhemko kuliko kawaida yaweza kuashiria kuwepo kwa matatizo ya kiakili na kisaikolojia
Uchunguzi na vipimo
Msichana yeyote aliyefikia umri wa kubalehe na kuvunja ungo na ambaye bado hajaanza kupata mabadiliko yeyote ya kubalehe katika mwili wake hana budi kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Aidha msichana aliyefikia umri wa miaka 16 na ambaye bado hajaanza kupata hedhi anatakiwa pia kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kwa wanawake waliokuwa wakipata hedhi kama kawaida lakini ghafla wakaacha kupata kwa muda wa miezi mitatu mfululizo au zaidi nao pia hawana budi kumuona daktari kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo hili.
Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanywa kuchunguza sababu za kukosa hedhi kwa mwanamke:
· Kupima damu kwa ajili ya kuchunguza kiwango cha homoni za FSH, LH, TSH na prolactin ambazo uzalishwaji wake unachochewa na tezi ya pituitary, na pia kupima kiwango cha homoni ya estrogen inayozalishwa na ovary.
· Kipimo cha ultrasound ya nyonga kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa matatizo katika njia ya uzazi na pia kuchunguza hali ya ovary.
· CT scan au MRI ya kichwa kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa matatizo kwenye tezi ya pituitary au hypothalamus.
· Vipimo vya kufahamu ufanyaji kazi wa tezi ya thyroid
· Kupima damu ili kufahamu kiwango cha homoni ya prolactin katika damu
· Kuchunguza uterus kwa kutumia aina ya X-ray inayoitwa Hysterosalpingogram na kipimo kingine kiitwacho Hysteroscopy ambacho huchunguza chumba cha uterus.
Matibabu ya kukosa hedhi
Matibabu ya kukosa hedhi yanaweza kufanyika nyumbani bila kuhitaji dawa, ingawa pia, kutegemeana na chanzo cha tatizo, yanaweza kuhitaji dawa na hata upasuaji wakati mwingine.
1. Matibabu yasiyohitaji dawa
o Baadhi ya wanawake wanaopata tatizo la kukosa hedhi kwa sababu ya kujinyima kula (wanaofanya dieting) na hivyo kupata upungufu wa virutubisho mwilini, wanashauriwa kula lishe bora.
o Baadhi ya wanawake wanaopata tatizo hili la kukosa hedhi kwa sababu ya kuongezeka uzito kupitiliza, wanashauriwa kuwa makini katika aina ya vyakula wanavyokula ili kuwa na uzito unaotakiwa.
o Wanawake wanaokosa hedhi kwa sababu ya kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi wanashauriwa kujiwekea kiasi katika ufanyaji wao wa mazoezi.
o Iwapo kukosa hedhi kumesababishwa na msongo wa mawazo, ni jambo jema kutafuta njia za kushughulikia matatizo hayo na kuyatatua ili kuondoa msongo wa mawazo
o Inashauriwa kutokuvuta sigara na kuacha kunywa kunywa pombe.
2. Matibabu yanayohitaji dawa: Matibabu ya kukosa hedhi hutegemea chanzo cha tatizo. Matibabu huelekezwa katika kutibu chanzo, na iwapo chanzo cha tatizo ni matatizo ya kimaumbile, upasuaji unaweza kufanyika. Kwa wanawake wenye matatizo ya kuwa na kiwango kingi cha prolactin, daktari anaweza kushauri matumizi ya dawa aina ya bromocriptine au pergolide. Kwa wanawake wenye upungufu wa homoni ya estrogen au wale wenye matatizo katika ovary zao, dawa zenye kurejesha homoni hiyo zaweza pia kutumika. Wakati mwingine dawa za uzazi wa mpango zaweza kutumika kurejesha mzunguko wa hedhi na pia kusaidia kuongeza kiwango cha homoni ya estrogen mwilini.
3. Upasuaji: Upasuaji unaweza kufanywa iwapo kuna
o Uvimbe katika ubongo unaoathiri tezi ya pituitary na hypothalamus
o Matatizo katika njia ya uzazi ya mwanamke
Je kukosa hedhi kunaweza kusababisha nisipate mtoto?
Ikumbukwe kuwa, kukosa hedhi si ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo tatizo hivyo basi iwapo tatizo hilo lina uhusiano na kutunga mimba na kupata mtoto, uwezekano wa kupata mtoto utakuwa mdogo ikiwa tatizo hilo halitashughulikiwa. Matatizo kwenye tezi za pituitary, hypothalamus pamoja na ovary ambayo yana uhusiano mkubwa na kukosa hedhi, husababisha pia tatizo la ugumba. Iwapo matatizo hayo yatashughulikiwa ipasavyo, uwezekano wa kupata kupata hedhi na hatimaye kupata mimba huwa mkubwa.
EmoticonEmoticon