Mwanamke anapopata ujauzito, mwili wake hupata mabadiliko yanayotokana na homoni mbalimbali zinazobadilika pale yai lake linaporutubishwa na mbegu za kiume. Mabadiliko haya huleta dalili mbalimbali ambazo huashiria ujauzito. Ingawa sio lazima mwanamke apate dalili hizi zote ili kuashiria ujauzito, anaweza akapata chache kati ya hizi;
Hii ni dalili ya mwanzo ya ujauzito. Kukosa hedhi kwa zaidi ya siku 10 toka siku ambayo mtu alikuwa anategemea kupata hedhi yake, huashiria kuwa ni mjamzito. Kukosa hedhi mwezi unaofuta huongeza zaidi uwezekano wa kuwa mjamzito. Ikumbukwe pia kukosa hedhi kunaweza kusababishwa na vitu vingine ukiacha ujauzito.
Baadhi ya wanawake wanaweza wakapata damu kidogo (vaginal spotting) kwa siku moja au mbili katika kipindi wanachotegemea hedhi. Hii inatokana na mimba kuwa inapandikizwa kwenye tumbo la uzazi. Damu huwa kidogo na hedhi huwa ya muda mfupi ukilinganisha na hedhi ya kawaida.
- Kichefu chefu na Kutapika
Hali ya kichefuchefu na kutapika hasa wakati wa asubuhi hujitokeza mwanzoni mwa ujauzito mpaka miezi mitatu au minne ya ujauzito. Hii huambatana na kukosa hamu ya kula baadhi ya vyakula. Kadri ujauzito unavyokua na hii hali hupungua. Huwapata zaidi ya theluthi mbili za wanawake wenye ujauzito. Kwa baadhi ya wanawake inaweza kuendelea wakati wote wa ujauzito.
- Kizunguzungu na Kichwa kuuma
Hali ya kizunguzungu hutokea kwa baadhi ya wanawake, hasa mwanzoni mwa ujauzito na kisha huaacha kadri mimba inavyoendelea kukua. Wakati mwingine inaweza kuambatana na kichwa kuuma. Mara nyingi ni hali ya mpito, na hivyo huacha baada ya muda.
Miezi ya mwanzo ya ujauzito huleta hali ya kukojoa mara kwa mara, na kuhisi mkojo hauishi. Hii inatokana na tumbo la uzazi kukandamiza kibofu cha mkojo wakati mimba inakua.
Hali ya mwili kuchoka hutokea sana mwanzoni mwa ujauzito, mara nyingi inatokana na mabadilikoya homoni ambayo mwili unaanza kuyapata kutokana na ujauzito.
Baadhi ya wajawazito hupata mabadiliko katika maziwa, yakiwemo kujaa na kuuma pale yanapoguswa. Mabadiliko ya kihomoni husababisha hali hii kutokea.
- Kununa au kukasirika ghafla na mara kwa mara (mood swings).
Kuna wajawazito hupata hii hali. Ni rahisi kukasirika ghafla na wakati mwingine kununa au kutojisikia furaha. Baadhi hufikia mpaka kiwango cha kuwanunia wenzi wao. Kwa hiyo hapo uvumilivu unahitajika kwa kweli!
Kadri muda unavyoenda, tumbo la mimba huwa linakuwa na kuanza kuonekana mara nyingi kuanzia miezi 3 ya ujauzito.
Dalili tulizoona mara nyingi huashiria ujauzito, lakini sio uthibitisho wa ujauzito. Hivyo ni muhimu kwenda hospitali uthibitishe kwa vipimo kwani kuna magonjwa ya mfumo wa uzazi yanayoweza kuleta dalili kama hizo. Vipimo vifuatavyo hufanyika kuthibitisha ujauzito:
- Kipimo cha Ujauzito cha Mkojo (Urinary Pregnancy Test).
Unaweza ukafanya kipimo hiki hospitali au mwenyewe ukinunua kwenye duka la dawa. Kipimo hiki kinaweza kupima ujauzito kuanzia wiki 2 toka mara ya mwisho kufanya mapenzi. Hupima homoni ya Human chorionic gonadotropin kwenye mkojo.
Ultrasound hufanyika kuthibitisha ujauzito, kama upo kwenye tumbo la uzazi na umri wa ujauzito. Kipimo hiki hufanyika hospitali.
Baada ya kuthibitisha ujauzito;
- Panga kituo cha afya na siku ya kuanza kliniki ya wajawazito ndani ya miezi 3 ya kwanza. Ukienda na mwenzi wako.
- Zingatia mlo kamili wakati wa ujauzito, soma hapa zaidi.
- Epuka kabisa unywaji wa pombe. Pata dondoo zaidi za afya wakati wa ujauzito hapa.
Share this
EmoticonEmoticon